Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mwl. Zainabu J. Makwinya ambaye pia ni Msimamizi wa Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa ameshiriki kama Mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mhe. Amir Mkalipa katika Ligi ya Mpira wa Miguu iliyoandaliwa na Diwani wa Kata ya Uwiro Mhe. Dauson Urio, Ligi iliyopewa jina la DIWANI CUP.
Ligi ya DIWANI CUP iliyofanyika leo tarehe 06 Oktoba,2024 ikiwa na lengo la kukuza michezo na kuhamasisha Wananchi kujitokeza kujiandikisha kwenye Daftari la Wakazi la wapiga Kura pamoja na kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Mkurugenzi Mtendaji na Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mwl. Makwinya amepata fursa kutoa elimu kwa wananchi wa Kata ya Uwiro kuhusu uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa kwa ngazi ya Mtaa na Kijiji pamoja na kueleza sifa za Kugombea na Kupiga Kura kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Mbali ya kutoa elimu hiyo, Msimamizi wa Uchaguzi na Afisa Uchaguzi Ndg. Edward Bujune wamegawa vipeperushi kwa wananchi vyenye maelezo yanayohusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa vikionyesha sifa za wagombea na wapiga kura pamoja na tarehe za kujiandikisha na tarehe ya Uchaguzi.
Hata hivyo, Katika uhamasishaji huo uliofanyika katika Kata ya Uwiro wananchi wamepatiwa elimu ya utofauti wa kujiandikisha kwenye daftari la Wakazi na Vitambulisho vya Kura vitakavyotumika kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani 2025.
Timu zilizoshiriki katika mashindano ya fainali ya DIWANI CUP ni Timu ya Kivumbi na Timu ya Kimulimuli ambapo Timu ya Kimulimuli imeibuka Kidedea kwa mikwaju ya Penati goli 4-3 baada ya Mchuano mkali wa dakika 90 bila kufungana.
Mhe.Diwani Kata ya Uwiro Dauson Urio kwa niaba ya Wananchi wa Kata ya Uwiro yenye vijiji vitatu vya Kisimiri Juu, Kisimiri Chini na Uwiro ametoa shukrani kwa Mkurugenzi Mtendaji kwa kufika na kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
"Serikali za Mitaa, Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi"
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa