Airtel Tanzania, kupitia programu yake ya "Shule Smart," imekabidhi vifaa vya Mtandao aina ya 'router' kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Mwl. Zainabu J. Makwinya, leo tarehe 5 Septemba 2024. Vifaa hivyo vinatarajiwa kusaidia kurahisisha usomaji kwa wanafunzi mashuleni.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Mwakilishi wa Airtel, Ndg. Harrison Isdory, amesema kuwa vifaa hivyo vitawawezesha wanafunzi kupata rasilimali mbalimbali za elimu kupitia tovuti za bure kama vile Tie Library na Shule Direct. Tovuti hizi zinatoa vitabu, mitihani iliyopita, na fursa ya wanafunzi kuuliza maswali na kupata majibu kwa haraka.
Mkurugenzi Makwinya, ameishukuru kampuni ya Airtel kwa msaada huo na kusisitiza kuwa vifaa hivyo vitachangia kuongeza kiwango cha ufaulu mashuleni. Aidha, amewataka Wakuu wa shule za Sekondari katika Halmashauri ya Meru kuweka usimamizi mzuri kwa wanafunzi mashuleni katika matumizi ya vifaa hivyo Ili kuboresha taaluma ya elimu.
Mkuu wa Shule ya Sing'isi, Mwalimu Datus Zabron, amesema kuwa vifaa hivyo vina umuhimu mkubwa katika elimu kwani vinapunguza mzigo wa Serikali wa kununua vitabu. Pia, ameeleza kuwa vifaa hivyo vinapanua wigo wa kujifunza na kuongeza maarifa kwa wanafunzi kwa kuwapa fursa ya kupata taarifa mbalimbali za masomo kwa njia ya mtandao, hivyo kuchangia katika kuongeza ufaulu mashuleni.
Halmashauri ya Wilaya ya Meru
Anwani: P.o. Box 462 Usa River
Simu ya Mezani: (+ 255) 272970482
Simu ya mkononi:
Barua pepe: ded@merudc.go.tz
Hakimiliki@2017 Halmashauri ya Wilaya ya Meru. Haki zote zimehifadhiwa