KLABU YA MICHEZO MERU YAIBUKA MSHINDI WA PILI KATIKA MASHINDANO YA KUADHIMISHA MIAKA 2 YA UONGOZI WA RAIS SAMIA
Imewekwa: November 17th, 2023
Na Annamaria Makweba
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mwl. Zainabu J. Makwinya leo amekabidhiwa kombe baada ya kupata ushindi wa nafasi ya Pili katika Mashindano ya kuadhimisha miaka miwili ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mapema Leo katika ofisi ya Mkurugenzi huyo, Mwenyekiti wa Klabu ya Michezo Halmashauri ya Wilaya ya Meru ( Meru DC Sport Club) Mwl. Moses Nathaniel Risasi amekabidhi kombe hilo baada ya timu hiyo kufika fainali na kupata ushindi wa pili na kupewa zawadi ya kombe.
Mashindano hayo yaliandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Vk. Mongella na kuanza katika viwanja tofauti tofauti huku kilele chake Kufanyika viwanja vya Sheikh Amri Abeid ambapo timu nane za Watumishi kutoka Halmashauri mbalimbali Mkoani Arusha zimeshiriki.
Aidha, Mwenyekiti wa Klabu hiyo Mwl.Moses Nathaniel Risasi amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kwa kuwawezesha kulipia gharama za usafiri na chakula kwa muda wote wa mashindano hayo.
Hata hivyo, ameeleza kuwa timu ya watumishi wa Halmashauri ya Meru ina mipango mikubwa ya kuinua michezo katika Halmashauri hiyo.