Katibu Tawala Mkoa wa Arusha(RAS) Missaile Albano Musa amefanya Ziara ya kukagua miradi ya Maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Meru .
Ziara hiyo imefanyika Leo ikiwa ni lengo la ufuatiliaji wa maelekezo ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John VK. Mongella, ambapo alitoa maelekezo ya marekebisho na maboresho katika baadhi ya miradi aliyotembelea hivi karibuni.
"Lengo la Ziara hii ni kufuatilia na kuona kama maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Mkuu wa Mkoa katika ziara yake yamefanyiwa kazi" Alisema RAS.
Kati ya Miradi aliyotembelea RAS ni pamoja na Shule Mpya ya Sekondari katika Kata ya Seela Sing'isi, Shule ya Msingi Leganga, Shule Mpya ya Msingi Nasholi pamoja na Shule ya Msingi Kaloleni.
Aidha, Katibu Tawala ametoa maelekezo kwa Kamati ya ujenzi katika Shule Mpya ya Sekondari Seela Sing'isi kuhakikisha Mradi huo unakamilika hadi kufikia tarehe 9 Disemba 2023 ili kufanya maandalizi ya kupokea wanafunzi katika shule hiyo ifikapo 2024.
Vilevile, RAS amekutana na Walimu katika shule zote alizotembelea na kusikiliza changamoto zao na kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji kuzifanyia kazi.
Kati ya changamoto zilizowasilishwa ni pamoja na Ombi la Ukarabati wa madarasa yaliyobaki katika shule ya Msingi Leganga, Choo cha Walimu, Upungufu wa Walimu na Uhaba wa Nyumba za Walimu katika shule ya Msingi Kaloleni hali inayosababisha Walimu kutoka mbali na kituo cha kazi.
Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Meru Mwl. Zainabu J. Makwinya ameeleza kuwa baadhi ya changamoto hizo zimeshaanza kufanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na shilingi Milioni 9,300,000.00 ambayo imetengwa kwa ajili ya ujenzi wa Choo cha Walimu katika shule ya msingi Leganga. Pia kuhusu suala la Ikama ya Walimu na Uhaba wa Nyumba za Walimu katika shule zilizotajwa ameahidi kulifanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuendelea kutenga bajeti.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Kaloleni Bw. Elias Mathayo Siria amekumbushia suala la ahadi ya kuwekewa Umeme katika shule hiyo ambapo TANESCO walitoa ahadi ya kumaliza tatizo hilo .